UTANGULIZI:
Bwana YESU asifiwe sana
wana wa MUNGU. Leo nina ujumbe ambao
unamuhusu kila mtu aliyeamua kuokoka na mwenye safari ya kwenda mbinguni. Yapo
mambo mengi sana ambayo kila mwamini anatakiwa kufanya na kuyafuata yaani
kuyaishi katika wokovu wake.
Tuangalie kwanza maana
ya “WOKOVU”
WOKOVU…Ni mpango wa
MUNGU wa kumtoa mwanadamu kutoka katika himaya ya shetani (chini ya nguvu za
giza) na kumuingiza katika himaya ya MUNGU kwa njia ya YESU KRISTO. (Wakolosai
1:13, Luka 1:78-79; Isaya 9:2)
Yesu Kristo alikuja
kutuokoa (Yohana 3:16) na wale wote waliomwamini wameokolewa yaani wameokoka.
(WARUMI 10:9).
Katika mtazamo wangu
nimeona yapo mambo manne ambayo ni ya lazima sana kwa kila mwamini. Mambo haya
ni kama yafuatayo:-
1 KUSOMA
NENO, KULITAFAKARI NA KULIISHI.
Hapa namaanisha kusoma
Biblia. Biblia ni nini?
Biblia ni mkusanyiko wa
vitabu ambavyo viliandikwa na watu wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Katika
kipengele hiki tutaangalia zaidi umuhimu wa kusoma neno la MUNGU au Biblia.
Kwanza kabisa naomba tutambue kuwa BIBLIA ni neno au sauti ya MUNGU.
Kila mwamini lazima awe
na ratiba yake ya kusoma neno la MUNGU katika maisha yake ya kila siku. Watu
wengi husoma Biblia hasa siku za ibada yaani Jumapili au siku ambazo
hukusanyika kwa ajili ya ibada. Sasa tuangalie baadhi ya umuhimu wa kusoma neno
la MUNGU (BIBLIA)
A NI MWONGOZO WA MAISHA YA KILA SIKU.
Katika maisha yetu ya
kila siku hasa wale tunaomwamini YESU kama mwokozi wetu, Biblia ndiyo mwongozo
wa maisha yetu. Kama ilivyo nchi kwmba ina mwongozo wake ambao ni katika, kumbe
hata sisi tunaweza kusema kuwa katiba yetu ya KIROHO ni BIBLIA. Kwa kusoma
Biblia ndipo utakapojua njia za kuendea au njia zipi usienende nazo ili usije
ukamkosea MUNGU wako.
ZABURI 119:11 Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.
Daudi alijua kabisa kwamba bila kuliweka neno
la MUNGU moyoni mwake basi katika kuishi kwake angekuwa anamkosea MUNGU. Kwa
hiyo ili uweze kuishi bila kukosea ni lazima uhakikishe unaliweka neno la MUNGU
ndani yako.
ZABURI 119:105 Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.
Neno la MUNGU Daudi kalifananisha kama taa ya
miguu yake. Kazi ya taa ni kumulika gizani ili kutoa Nuru uweze kuona hata kama
kuna shimo huwezi kutumbukia. Kwa hiyo Biblia pia inatupa mwanga ili wa jinsi gani uweze kuenenda katika
maisha yako ya kila siku.
2Timothy 3:16 Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza,
na kwa kuwaadibisha katika haki
B. NI CHAKULA CHA ROHO.
Binadamu ana ROHO na
MWILI. Ili mwili uweze kuishi lazima mtu ale chakula na ndiyo maana tunakula
chakula kila siku hadi milo mitatu. Kama mwili unalishwa vivyo hivyo hata roho
inatakiwa ile ili iweze kukua. Sasa chakula cha ROHO ni NENO la MUNGU yaani Biblia.
Mtu ambaye hasomi neno la MUNGU hawezi kukua kiroho. Kukua kiroho ni ile hali
ya kuongezeka katika kuyajua mambo ya MUNGU na kulitendea kazi.
1Peter 2:2 Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa
yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;
Baada ya kuokoka na kubatizwa kwa Roho
Mtakatifu unakuwa umezaliwa mara ya pili. Chochote kinachozaliwa lazima kipate
chakula ili kiweze kukua. Sasa kuna watu walizaliwa mara ya pili lakini
wakakosa chakula matokeo yake wameugua kwashakoo ya kiroho/wamedumaa na siku
zote wamebaki kuwa kama watoto. Hii inasababishwa na wao kutokula chakula
ambacho ni neno la MUNGU.
C. NI SILAHA DHIDI YA ADUI
Silaha ni kifaa au kitu
kinachotumika katika kujilinda na
maadui. Wapo maadui wa aina mbili kama vile tulivyoona hapo juu kuwa kuna mwili
na roho; kuna maadui wa mwili na maadui w kiroho. Maadui wa kimwili unapamba
nao kwa silaha za mwili. Pia maadui wa kiroho unaambana nao kiroho. Hapa
nitazungumzia kwa habari ya silaha za kiroho tu maana neno la MUNGU linasema
katika Warumi 8:14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndiyo
wana wa Mungu. Kama mtu
akiongozwa na roho ina maana hata katika kuenenda ni kiroho. Kwa hiyo vita yetu
haipo katika mwili wa damu na nyama, bali katika ulimwengu wa roho kama Waefeso 6:12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya
damu na nyama; bali ni juu ya
falme na mamlaka, juu ya
wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
WAEFESO 6:13-17
Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu,
mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni,
na kuvaa dirii ya haki kifuani,
na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili
ya amani;
zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo
kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa
Roho ambao ni neno la Mungu.
Ukiangalia mstari wa 17 unasema neno la MUNGU
ni upanga wa Roho. Kazi ya upanga ni kukata vitu. Kwa hiyo kama ni upanga wa
Roho basi yale mambo ambayo yanaletwa na adui shetani yanakatwa na neno la
MUNGU.
Waebrania 4:12 Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu,
tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta
yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
2 MAOMBI.
Maombi ni
mazungumzo kati ya mwanadamu na MUNGU.
Tunawasiliana na MUNGU kwa njia ya maombi. Kila aliyemwamini YESU kama Bwana na
mwokozi wa maisha yake, automatically ni kwamba anamwamini MUNGU wa mbinguni
aliyeziumba mbingu na nchi. YOHANA 15:23 Yeye anichukiaye mimi humchukia na Baba yangu. Mungu anapenda sana ushirika wa Karibu na watu wake anapenda awe anasemezana nasi kila
iitwapo leo na kumshirikisha katika kila jambo ndiyo maana anasema katika WAFILIPI 4:6 Msijisumbue kwa neno lo lote; bali
katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.
Yani kila shida ulinayonayo MUNGU anataka aijue
aweze kukusaidia. MUNGU yeye ni Baba yetu ndiyo maana anataka atusaidie
mahitaji yetu. Mtoto siku zote husaidiwa na Baba yake. Kwa njia ya maombi ndipo
unapoweza kumweleza MUNGU shida zako wala siyo njia nyingine.
MITHALI 3:5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala
usizitegemee akili zako mwenyewe;
Angalia hapa YESU anavyosisitiza YOHANA 16:24 Hata sasa hamkuomba
neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu. Hapa alikuwa anawambia wanafunzi wake
waombe.
Maombi ni ya msingi sana mwana wa MUNGU. Yapo
mambo ambayo hayawezi kufanyika kwako bila kuwa mwombaji. Hili tunaliona pia
wakati wanafunzi wa YESU wameshindwa kutoa pepo akawambia katika MATHAYO 17:21 Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na
kufunga.
3 UTAKATIFU.
Utakatifu ni kuishi
maisha ya kumpendeza MUNGU. Ni maisha ambayo
mtu anaishi kwa kufuata taratibu
zote za ki-MUNGU huku akiongozwa na neno La MUNGU yaani Biblia. Mtu yeyote anayetembea
katika utakatifu aba sifa zifuatazo:-
a)
Ni mcha MUNGU.
b)
Anatii NENO la MUNGU, watumishi pamoja
raia wengine.
c)
Ni mnyenyekevu wa Roho.
d)
Yuko tayari kukosolewa.
e)
Siyo mtu wa hasira.
f)
Ni mtu mwenye furaha na ana upendo kwa
watu wote.
g)
Huitafakari sheria ya MUNGU wakati wote.
4 KUWALETA
WENGINE KWA YESU.
Hapa nazungumzia
kuhubiri habari njema za mwokozi YESU kwa mataifa yote. MUNGU anapenda sana
sisi tufanye kazi ya kumnyang’anya shetani watu kwa njia mbali mbali. Na hili
ni agizo alilitoa YESU mwenyewe katika MATHAYO 28: 19 Basi, enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana,
na Roho Mtakatifu;
20 na kuwafundisha
kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku
zote, hata ukamilifu wa dahari.
Waamini wengi wamekuwa
hawatii agizo hili. Hii inatokea kwa sababu wanafikiri kazi ya kuhubiri habari
njema ni ya Wainjilisti tu au wachungaji. Tukisoma hayo maandiko hayakusema
watu flani bali waliambiwa wote. Kila mtu aliyeokoka ni Mtumishi wa MUNGU na
ana jukumu la kuhakikisha anaongeza wafuasi wa YESU kwa kuwahubiri kwa matendo
yake pamoja na kuwafuata mataifa na
kuwambia habari njema za YESU KRISTO. MUNGU yeye alitupenda sana hata akamtoa
YESU afe kwa ajili yetu. Na sisi inatakiwa tuwe na upendo kwa ndugu, jamaa na
rafiki zetu kwa kuwambia furaha na uzima uliopo watakapomwamini YESU.
Tusiwaachie tu wachungaji jukumu hili bali kila mmoja awajibike kwa jinsi MUNGU
atakavyomuwezesha. Kama huwezi kuhubiri basi shiriki katika kazi hii hata kwa
kutoa mali zako.
YESU anasema katika
MATHAYO 12:30 Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na
mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.
YESU alikuja ili kuwaokoa watu kutoka katika
dhambi, shida, adha, mateso na vifungo mbali mbali. Sasa kama mtu wa MUNGU
hushiriki katika kuyatenda hayo ina maana unatapanya. Maana kwa sasa watenda
kazi ni sisi yeye alindoka akatuachia agizo ya kuiendeleza kazi hii.
Bwana YESU anasema katika Luke 10:2 Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi
katika mavuno yake.
Kuna watu wengi sana huko duniani wanateseka
sana, adui shetani anawatumikisha katika dhambi, wameshindwa kutoka kwa sababu
hata watu wa kuweza kuwatoa hawapo. Ndiyo maana akasema watenda kazi ni
wachache. Lakini mimi na wewe tunao uwezo wa kuifanya kazi ya BWANA ya kuvuna
endapo tutaamua kujitoa kwa dhati kama wale Mitume walivyoweza kujitoa.
Asanteni sana.
No comments:
Post a Comment